+255 659 215 984
 info@limaplatform.co.tz

MBINU ZA UFUGAJI SAMAKI KISASA

                        

UTANGULIZI

 Ingawa samaki amezoeleka kuwa wanaishi wenyewe huko porini(majini) bila kufugwa na mtu bado samaki anaweza kufugwa kama mifugo mingine. Samaki anaweza kutengenezewa mazingira kama yale ya porini na Akaishi vizuri.Hitaji kubwa la Samaki ili aishi ni maji na chakula.Kwa hiyo unaweza kuchimba mabwawa au kutumia vizinga kufuga Samaki.Samaki aina ya Kambale na Perege ni Samaki wanaopendwa  sana kufugwa nchini Tanzania.

FAIDA ZAKUFUGA SAMAKI

1. Kuhakikisha Samaki wanapatikana bila kujali mabadiliko ya tabia ya nchi.

2. Kuhakikisha taifa linapata chakula na kuondokana na utapiamlo.

3. Kupunguza Maadui wa samaki mfano kenge na vyura

4. Unaweza kuzalisha wakati wowote unaohitaji na kwa idadi unayohitaji .

5. Samaki wa kufugwa anakuwa na uzito mkubwa

           VITU VYA KUZINGATIA UNAPOTAKA KUFUGA SAMAKI

  1. UCHAGUZI WA ENEO

Hii ni hatua muhimu sana kwa mkulima,Kuchagua eneo ambalo lina sifa stahiki za kuchimba bwawa. Uchaguzi mzuri wa eneo utakuwezesha kupata matokeo mazuri katika ufugaji wako.Unapochagua eneo hakikisha eneo hilo lina sifa zifuatazo ,

  1. Lisiwe ni eneo lenye historia ya kuwa na mafuriko.
  2.  Eneo ambalo upatikaji wa maji ni wa uhakiki na kwa wingi mwaka mzima.
  3.   Liwe na mwinuko kidogo na lisiwe tambalale,likiwa tambarare nirahisi kusombwa na mvua kubwa zikitokea.
  4. Chunguza aina ya udongo uliopo kwa msaada wa wataalam ili kujua utumie njia gani kuhakikisha maji yanatuama vizuri katika bwawa lako. Udongo wenye uwezo mkubwa wa kutunza maji ni udongo aina ya mfinyazi.Katika kila aina ya udongo kuna namna ya uchimbaji wa bwawa.
  • UCHIMBAJI WA BWAWA

Kanuni za ujumla za kuchimba bwawa ni kama ifuatavyo,

i.Haishauliwi kuchimba bwawa kubwa sana kurahizisha uhuudumiaji.Pia inashauriwa bwawa wako liwe na umbo la mstatiri kurahisisha namna utakavowahudumia.

ii.Unapochimba bwawa lako hakikisha  kingo za bwawa zimeegemee nje ili kuzuia  mmomonyoko wa udongo na kurudi tena ndani ya bwawa.

iii.Uchimbaji wa bwawa unategemea sana aina ya udongo uliopo katika eneo hilo.Hivyo ni vizuri kushirikiana na wataalamu ili kujua aina ya udongo kabla ya kuanza  kuchimba bwawa.

Kuna aina kuu tatu za udongo

i.Tifutifu

ii.Mfinyazi

iii.Mchanga

Uchimbaji wa bwawa katika udongo wa mfinyazi.

Huu udongo hauna shida sana kwa sababu ni mzuri sana kwa kutuamisha maji.Kabla ya kuanza kazi ya kuchimba hakikisha eneo lote limesafishwa vizuri kama kuna visiki na aina yoyote ya miti imetolewa.Wakati wa kuchimba bwawa ni muhimu liwekwe  kingo.Kingo za bwawa hazitakiwi kusimama wima bali lazima zilale kwa kiasi ili kuzuia mmomonyoko wa udongo.Kingo zilizosimama zinafyonza haraka maji na kusababisha uzito mkubwa unaoweza kubomokea ndani ya bwawa,lakini kingo zilizolala hufyonza maji taratitibu sana na ni vigumu kubomokea ndani.Ulalo wa ardhi unaweza kufanana na paa la nyumba.

Kingo za bwawa lazima zishindiliwe vizuri.Hakikisha bwawa lako limewekwa sehemu za kuingizia maji na kutolea maji ili kurahisisha zoezi la kubadilisha maji.Baada ya hatua  hizo jaza maji kwenye bwawa lako,Rutubisha bwawa lako na litakuwa tayari kwa ajili ya kuweka Samaki. Na kisha unaweza kupanda majani kwenye kingo za bwawa ili kuimarisha kingo za bwawa.

          

Uchimbaji wa bwawa katika eneo ambalo siyo la mfinyazi.

Hatakama eneo halina udogo wa mfinyazi lakini bado linaweza kuchimbwa bwawa na likazalisha Samaki vizuri kabisa. Kwa ardhi isiyohifadhi maji baada ya bwawa kumalizika kuchimbwa ni muhimu liwekewe karatasi ya plastiki ili kupunguza kasi ya upoteaji wa maji. Baada ya kumaliza kuchimbwa na kukamilika kabisa, karatasi hizo hulazwa vizuri na kuwekewa udongo kidogo ili kuzuia karatasi lisitoke na kuruhusu mimea midogo sana kuota.Hatua inayofuata ni upandaji wa majani kwenye kingo za bwawa nah apo bwawa lako litakuwa tayari.

Katika udongo huu pia unaweza kujenga bwawa kwa kupiga plasta ili kuzuia upotevu wa maji. Baada ya kuchimba bwawa lako vizuri na kuweka sehemu za kutolea na kuingizia maji, unaweza kujenga kuta zake kwa sement , hakikisha bwawa lote limepigwa niru kabisa ili kuzui chembechembe za siment kubaki kwenye bwawa. Baada ya hapo utajaza maji ya kwanza na kuyamwaga tena baada ya siku kadhaa ili kuondoa sumu ya sementi. Halafu utajaza tena maji mengine tena kwa ajili ya kuanza ufugaji.

Zingatia: Unaweza kupiga plasta pia kwenye udongo wa mfinyazi na bwawa lako na likawa vizuri.

    3.  KURUTUBISHA BWAWA

Robo tatu ya chakula cha samaki ni uoto wa mimea usioonekana kwa macho ambaohuzalishwa baada ya bwawa kurutubishwa. Bwawa hurutubishwa kwa kuwekwa mbolea za wanyama kama ngombe,mbuzi na kondoo.  Mbolea inafungwa kwenye mfuko kwa kiwango maalumu na kuwekwa kwenye bwawa kwa muda wa siku saba kisha ukijani utatokea.Kama bwawa ni sementi baada ya siku saba utatoa hayo maji na kujaza mengine tena. Ila kama bwawa lako siyo la kujengwa na simenti unaweza kupanda Samaki wako. Muonekano wa maji yako utabadilika kuwa kama picha inavoonyeshwa na litakuwa tayari kupandwa Samaki.

4. KUSAFIRISHA VIFARANGA

Ni vizuri vifaranga vikasafirishwa kwa kutumia mifuko ya nailon au makontena kuruhusu hewa kupita. Pia vifaranga vikisafirishwa asubuhi inakuwa vizuri sana. Idadi isiwe kubwa sana ili kuruhusu hewa kupita.

5. CHAKULA NA JINSI YA KULISHA

Chakula cha kwanza cha samaki ni kile kilichozalishwa. Na kingine hutengenezwa na wataalam. Kwa kila hatua Samaki hulishwa chakula cha aina yake.Kuna chakula cha ungaunga kwa Samaki wadogo sana lakini wale walioongezeka mara nyingi wataalamu wanashauri wapewe pellet. Samaki hulishwa mara mbili kwa siku kwa kiwango maalumu baada ya kufuata maelekezo ya mtaalamu. Mtaalamu atakusaidia kujua uzito wa Samaki na kiwango wanachohitaji kwa siku. Ni muhimu kutenga eneo maalumu la kulishia na muda maalumu,Samaki kama viumbe hukariri muda wao wa kula.

6. JINSI YA KUTUNZA BWAWA

Ni muhimu kufyeka maeneo yanayozunguka bwawa ili kuwazuia maadui wa Samaki kama kenge na Vyura. Vyura hupenda kula mayai ya samaki. Pia ni muhimu kulichunguza bwawa lako na  kubadilisha maji  pale unapoona utofauti ili kuoondoa uchafu na kuruhusu mwendelezo wake.

7. UVUNAJI WA SAMAKI

 Samaki huvuliwa kuanzia ifikapo miezi sita. Mfano sato ifikapo miezi sita anakuwa amefikisha uzito usiopungua 350 gramu.